Wednesday, October 22, 2014

Katiba pendekezwa na Sanaa Tanzania

Leo nizisogeze karibu nanyi wasanii na wasomaji wa blog hii zile ibara tatu ambazo zimejikita kwa namna moja au nyingine kwenye sanaa. Ni vyema kuzipitia na kuzifahamu ili kutoka hapa tujipange vyema kuhakikisha kuwa sheria nzuri zinatungwa ili kuzaa matunda yenye faida kwa wasanii na wananchi kwa ujumla. Ibara hizi ni kama ifuatavyo:

Ibara ya 15: Lengo la taifa kiutamaduni
(1) Lengo la Katiba hii kiutamaduni ni kukuza, kudumisha na kuhifadhi lugha ya Kiswahili, urithi wa asili na utamaduni wa wananchi.
(2) Katika kuhakikisha utekelezaji wa lengo hilo, Serikali itachukua hatua zinazofaa ili:
(a) kulinda na kuendeleza lugha ya Kiswahili;
(b) kulinda na kuhifadhi urithi wa asili, malikale na sehemu zenye umuhimu wa kihistoria ili kuepuka uharibifu, wizi au utoroshaji nje ya nchi;
(c) kulinda, kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa jamii mbalimbali; na
(d) kujenga utamaduni wa kuwepo ushirikiano, maelewano, maridhiano, uvumilivu na kuheshimu mila, desturi na imani ya dini ya kila mtu.

Ibara ya 39: Uhuru wa maoni
Kila mtu:
(a) Ana haki na uhuru wa:
(i) kuwa na maoni na kueleza fikra zake;
(ii) kufanya mawasiliano na kutoingiliwa katika mawasiliano yake; na
(iii) kufanya ugunduzi, ubunifu na utafiti wa sanaa, sayansi na mapokeo ya asili.

Ibara ya 59: Uhuru wa taaluma, ubunifu, ugunduzi, na usanii
(1) Kila mtu atakuwa na uhuru wa kushiriki kwenye mambo yanayoendeleza na kukuza sanaa, taaluma, ubunifu na ugunduzi.
(2) Kila mtu atakuwa na uhuru wa kujifunza, kufundisha, kutafiti na kueneza matumizi ya matokeo ya utafiti kulingana na kanuni za kitaaluma na za kiutafiti.
(3) Serikali itakuza na kuendeleza utafiti, ubunifu na ugunduzi katika sanaa, sayansi na teknolojia kwa kutunga sheria ambazo:
(a) zitalinda hakimiliki na hataza na haki za wabunifu, watafiti na wasanii;
(b) zitawezesha taasisi za elimu na za utafiti kutumia ugunduzi wao kwa manufaa ya Taifa;
(c) zitasimamia uhamishaji wa sayansi na teknolojia;
(d) zitawezesha kukuza rasilimali watu kwenye nyanja za kitaaluma, sayansi, teknolojia na ubunifu;
(e) zitalinda na kusimamia ubora wa taaluma, utafiti na matumizi ya ugunduzi na ubunifu; na
(f) zitafafanua mambo mengine yanayohusu hakimiliki na hataza.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...