Saturday, September 27, 2014

Kituo cha watoto wasioona - Shinyanga


Katika kumuenzi Marehemu Mzee Felix Ngelela Luhende wa Shinyanga anapofikisha miaka minne (4) tangu mauti yake; familia yake ikiongozwa na Mama Hildegard Felix Luhende ilijitoa na kusaidia watoto wasioona, wasiosikia na watoto wenye ulemavu wa ngozi wa kituo cha Blinds kilichopo Buhangija - Shinyanga kwa kuweka plasta na sakafu katika upande mmoja wa bweni moja ambalo lilikuwa halijamaliziwa na bado halitumiki ipasavyo.
Bweni lililowekewa plasta na sakafu
Bweni kabla ya ujenzi wa plasta na sakafu
Bwenini: Ujenzi ukiendelea
Bwenini: Baada ya ujenzi kukamilika
Mpaka siku ya terehe 21/09/2014 kituo kilikuwa kina watoto 276 ambao wanachangia mabweni matatu; la nne likiwa ndio hilo ambalo halijakamilika. Mabweni haya bado hayawatoshi watoto wote kwa pamoja. Hii huwalazimu watoto hao kulala wawili wawili mpaka wanne wanne kwenye kitanda kimoja.
Hivi ni vitanda ambavyo walemavu hulala wawili wawili mpaka wanne
 Ili watoto waweze kuyatumia mabweni haya kwa ufasaha bweni mmoja lina uwezo wa kuwahifadhi watoto 48 lakini kwa hali ya sasa bweni mmoja hubeba watoto 75 mpaka 80 na zaidi, jambo ambalo huwatisha walezi hasa wakifikiria magonjwa ya mlipuko.

Hii iliwafurahisha sana watoto wakitazamia muda si mrefu wengine kuhamia humo na hivyo kupunguza kujaa kwenye mabweni mengine.
Zaidi ya hapo familia ya Mzee Felix Luhende pia iligundua watoto hao walikuwa hawana mahala pa kuanika nguo zao ambapo walilazimika kuanika nguo hizo kwenye madirisha, hivyo familia ikaona ni vema kuwawekea watoto hao kamba kadhaa za kuanikia nguo zao.

Chuma za kufungia kamba za kuanikia nguo zikisubiriwa kukauka
Kituo bado kinahitaji sana misaada mingi kama vile kusaidia kuboresha jiko lao ili kuruhusu hewa zaidi kuingia ndani, kuboresha bwalo lao, kuongeza vitanda na magodoro, chakula na kadhalika. 
Zaidi ya hapo walezi wanahitaji mafunzo zaidi ya malezi na usimamizi ili kuboresha baadhi ya mambo ya msingi katika kuwalea watoto hao.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...