Tuesday, March 3, 2015

Filamu fupi ya 'KOSA' yaingia production.

Mwongoza na mtayarishaji mahiri wa Filamu hapa nchini Edgar Ngelela anatarajiwa kuachia filamu mpya fupi iliyopewa jina la ‘KOSA’ mwanzoni mwa mwezi wa nne mwaka huu.

Filamu mpya ya 'KOSA'
Ngelela ambaye filamu yake ya awali ya ‘Anguko’ ilipata mafanikio makubwa ya kuoneshwa katika tamasha la kimataifa la 16 la majahazi (ZIFF) huko Zanzibar mwaka 2013, ameiambia Radio Mlimani kwamba filamu hiyo fupi ya ‘KOSA’ inatarajiwa kuwa na urefu wa dakika 25 ikizungumzia maisha ya kila siku.

“Maudhui ya filamu yangu mpya ni maisha ya kila siku lakini zaidi inagusa mapezi, imani na mazoea” alisema Ngelela wakati akizungumza na Radio Mlimani juu ya ujio wa filamu hiyo mpya.

Ngelela ameamua kuiita filamu hiyo ‘KOSA’. Neno hilo la Kiswahili limeubeba ujumbe wa filamu hiyo ipasanyo; kwanza limetumika katika filamu hii likimaanisha kukosa, lakini pia limetumika likimaanisha kukosea, hivyo basi neno hilo limebeba mambo yote mawili katika filamu hiyo fupi, Ngelela alisema.

“Filamu hii ni filamu inayotoa ujumbe kwamba kama mwanadamu ni lazima uwe makini katika kufanya maamuzi, lakini pia kuwaambia watanzania kwamba kila mahusiano ya kimapenzi yana upekee wake” alimalizia mtayarishaji huyo.

Filamu hiyo itakayokamilika mwanzoni mwa mwezi wa nne imelengwa kuoneshwa katika matamasha mbalimbali ya kimataifa na vile vile itapatikana katika DVD hapo baadae.

Miongoni mwa nyota wa filamu hapa nchini waliongára katika filamu hiyo ni pamoja na Bi Madina Hamis maarufu kama dada zawadi pamoja na Emmanuel Myamba anayejulikana zaidi kama Pastor Myamba. Wapo pia waigizaji chipukizi ambapo kwa mujibu wa Ngelela wamefanya kazi kubwa katika filamu hii.

Filamu hiyo imechezewa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na pia katika viunga vya mji wa Morogoro.


Na Sylvia Mwehozi, Radio Mlimani.

No comments:

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...