Mwongoza na mtayarishaji mahiri wa Filamu hapa nchini Edgar Ngelela anatarajiwa kuachia
filamu mpya fupi iliyopewa jina la ‘KOSA’ mwanzoni mwa mwezi wa nne mwaka huu.
Filamu mpya ya 'KOSA' |
Ngelela
ambaye filamu yake ya awali ya ‘Anguko’ ilipata mafanikio makubwa ya kuoneshwa
katika tamasha la kimataifa la 16 la majahazi (ZIFF) huko Zanzibar mwaka 2013,
ameiambia Radio Mlimani kwamba filamu hiyo fupi ya ‘KOSA’ inatarajiwa kuwa na
urefu wa dakika 25 ikizungumzia maisha ya kila siku.
“Maudhui
ya filamu yangu mpya ni maisha ya kila siku lakini zaidi inagusa mapezi, imani
na mazoea” alisema Ngelela wakati akizungumza na Radio Mlimani juu ya ujio wa
filamu hiyo mpya.
Ngelela
ameamua kuiita filamu hiyo ‘KOSA’. Neno hilo la Kiswahili limeubeba ujumbe wa
filamu hiyo ipasanyo; kwanza limetumika katika filamu hii likimaanisha kukosa,
lakini pia limetumika likimaanisha kukosea, hivyo basi neno hilo limebeba mambo
yote mawili katika filamu hiyo fupi, Ngelela alisema.
“Filamu
hii ni filamu inayotoa ujumbe kwamba kama mwanadamu ni lazima uwe makini katika
kufanya maamuzi, lakini pia kuwaambia watanzania kwamba kila mahusiano ya kimapenzi
yana upekee wake” alimalizia mtayarishaji huyo.
Filamu
hiyo itakayokamilika mwanzoni mwa mwezi wa nne imelengwa kuoneshwa katika
matamasha mbalimbali ya kimataifa na vile vile itapatikana katika DVD hapo
baadae.
Miongoni
mwa nyota wa filamu hapa nchini waliongára katika filamu hiyo ni pamoja na Bi
Madina Hamis maarufu kama dada zawadi pamoja na Emmanuel Myamba anayejulikana
zaidi kama Pastor Myamba. Wapo pia waigizaji chipukizi ambapo kwa mujibu wa Ngelela
wamefanya kazi kubwa katika filamu hii.
Filamu
hiyo imechezewa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na pia katika viunga
vya mji wa Morogoro.
Na Sylvia
Mwehozi, Radio Mlimani.